Thursday, February 17, 2011

RAMBIRAMBI

 
RAMBIRAMBI
 
Kwa niaba ya Tanzanian Canadian Association (TCA), chama cha jumuiya ya Watanzania tunaoishi Toronto , Ontario , Canada na vitongoji vyake, tunapenda kuchukua fursa hii kwanza kabisa, kutoa rambirambi zetu kwa familia za wananchi waliopoteza wapendwa wao katika ajali ya mabomu yaliyolipuka katika kambi ya jeshi eneo la Gongo La Mboto, Dar-es- Salaam , Tanzania .
 
Tunawaombea wote waliopoteza maisha yao Mwenyezi Mungu awapumzishe kwa amani; tunawatakia majeruhi waugue pole, wapone haraka ili waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku. Vilevile, tunawatakia wote waliopotezana na ndugu zao hususan watoto waliopotezana na wazazi wao waweze kupatikana na kukutana tena.
 
Tumesikitishwa na taarifa za maafa hayo na kuhuzunishwa kuona kwamba ni mara ya pili tukio kama hili linatokea nchini kwetu. Wengi watakumbuka siku si nyingi janga kama hili lilitokea kule Mbagala. Tunapenda kuuomba uongozi wa jeshi uangalie upya namna silaha kali zinavyohifadhiwa; katika utaratibu wa kuhifadhi mabomu, tunapendekeza yafanyike marejeo na marekebisho yatakayozingatia usalama wa raia.
 
Katika kuhitimisha, tunalisisitizia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), lichukue hatua madhubuti na za haraka katika kuhakikisha majanga yanayoweza kuepukika kama haya hayatokei tena.
 
Mungu Ibariki Tanzania .
 
Uongozi – Tanzanian Canadian Association (TCA)
 
 

No comments: