Sunday, November 28, 2010

REAL MADRID FC KUPAMBANA NA BARCELONA FC -KESHO

Lile pambano linalosubiriwa kwa hamu la miamba ya soka nchini Hispania,Real Madrid na Barcelona, limewadia. Zikiwa zimebakia saa chache wachezaji wa pande zote mbili wanaashiria kutoogopa timu pinzani au mpambano huo kwa ujumla.
Real Madrid chini ya kocha Jose Mourinho, inaingia kwenye pambano hilo ikiwa haijapoteza mchezo kwa kushinda mechi kumi na sare mbili.Kwa upande wa Barcelona wao wana rekodi ya kushinda mechi kumi sare moja na kupoteza mchezo mmoja.
Kukiwa hakuna majeruhi kwa pande zote mbili, mpambano huo unatarajiwa kuwa mkali kwani kumbukumbu zinaonyesha, toka walipokutana kwa mara ya kwanza mwaka 1902, Madrid imeshinda mara 85 na Barcelona 81 huku kukiwa na sare 42.
Mchezaji nyota wa Real Madrid, Christiano Ronaldo amesema wao wanakwenda Camp Nou kwa nia ya kutafuta ushindi na si vinginevyo wakati Lionel Messi,mshambuliaji hatari wa Barcelona, raia wa Argentina, alikaririwa akisema hivi karibuni kwamba Barcelona bado ni timu bora kuliko wapinzani wao, ingawa anakubali kuwa bidii na moto wa Madrid mwaka huu ni tofauti na misimu miwili iliyopita.
Mourinho anatarajia kupunguza “uteja” wa Madrid kwa Barcelona chini ya Guardiola, wakati Mourinho akitamba kuujua mpambano huo hata akiwa usingizini.Madrid hawajaifunga Barcelona nyumbani toka desemba ya 2007 na Mourinho ameshaifunga Barcelona akiwa kocha wa Chelsea na Inter Milan.Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa kocha Jose Mourinho kuiongoza Real Madrid katika mpambano na Barcelona.
Ushindi katika El Classico unachukuliwa kuwa ni ishara ya ushindi wa ligi kwani katika misimu sita iliyopita, mshindi wa mpambano huu ndiye aliyechukua kombe mwisho wa msimu.Jumla ya mashabiki 98,000 wanatarajiwa kushuhudia mpambano huo ndani ya Uwanja wa nyumbani wa Barcelona,Nou Camp,huku mamilioni ya mashabiki wa soka ulimwenguni wanatarajiwa kuufuatilia mpambano huo kupitia luninga na mtandaoni.

Nyota wa pande zote mbili wamekuwa na ari ya kutaka kuonyesha vipaji na uwezo wao wakati Ronaldo na Messi wakimimina mvua za magoli katika mechi za karibuni.Huu unaaminika kuwa pia mpambano baina ya Ronaldo na Messi katika kuonyesha nani ni bora zaidi miongoni mwao.
Zote hizi ni dondoo tu, mpira huchezwa kwa dakika tisini.Tusubiri matokeo.
Written by E.Manambi with additional notes by Jeff Msangi


No comments: